Luke 17

Isa Afundisha Kuhusu Majaribu, Dhambi Na Imani

(Mathayo 18:6-7, 21-22; Marko 9:42)

1 aIsa akawaambia wanafunzi wake, “Mambo yanayosababisha watu watende dhambi hayana budi kutukia. Lakini ole wake mtu yule anayeyasababisha. 2 bIngekuwa heri kama mtu huyo angefungiwa jiwe la kusagia shingoni na kutoswa baharini, kuliko kumsababisha mmojawapo wa hawa wadogo kutenda dhambi. 3 cKwa hiyo, jilindeni.

“Kama ndugu yako akikukosea mwonye, naye akitubu, msamehe.
4 dKama akikukosea mara saba kwa siku moja na mara saba kwa siku moja akaja kwako akisema, ‘Ninatubu,’ msamehe.”

Imani

5 eMitume wake wakamwambia Bwana, “Tuongezee imani.”

6 fBwana akawajibu, “Kama mkiwa na imani ndogo kama punje ya haradali, mngeweza kuuambia mti huu wa mkuyu, ‘Ng’oka ukaote baharini,’ nao ungewatii.

Wajibu Wa Mtumishi

7“Ikiwa mmoja wenu ana mtumishi anayelima shambani au anayechunga kondoo, je, mtumishi huyo arudipo atamwambia, ‘Karibu hapa keti ule chakula?’ 8 gJe, badala yake, hatamwambia, ‘Niandalie chakula, nile, jifunge unitumikie ninapokula na kunywa; baadaye waweza kula na kunywa?’ 9Je, huyo mtu atamshukuru mtumishi huyo kwa kutimiza yale aliyoamriwa? 10 hVivyo hivyo nanyi mkiisha kufanya mliyoagizwa, semeni, ‘Sisi tu watumishi tusiostahili; tumefanya tu yale tuliyopaswa kufanya.’ ”

Isa Atakasa Wakoma Kumi

11 iIsa alipokuwa njiani akienda Yerusalemu, alipitia mpakani mwa Samaria na Galilaya. 12 jAlipokuwa akiingia kwenye kijiji kimoja, watu kumi waliokuwa na ukoma wakakutana naye. Wakasimama mbali, 13 kwakapaza sauti, wakasema, “Isa, Bwana, tuhurumie!”

14 lAlipowaona akawaambia, “Nendeni mkajionyeshe kwa makuhani.” Nao walipokuwa njiani wakienda, wakatakasika.

15 mMmoja wao alipoona kwamba amepona, akarudi kwa Isa, akimsifu Mungu kwa sauti kuu. 16 nAkajitupa miguuni mwa Isa akamshukuru. Yeye alikuwa Msamaria.

17Isa akauliza, “Je, hawakutakaswa wote kumi? Wako wapi wale wengine tisa? 18Hakuna hata mmoja aliyeonekana kurudi ili kumshukuru Mungu isipokuwa huyu mgeni?” 19 oIsa akamwambia, “Inuka na uende zako, imani yako imekuponya.”

Kuja Kwa Ufalme Wa Mungu

(Mathayo 24:23-28, 37-41)

20 pIsa alipoulizwa na Mafarisayo Ufalme wa Mungu utakuja lini, yeye akawajibu, “Ufalme wa Mungu hauji kwa kuchunguza kwa bidii, 21 qwala watu hawatasema, ‘Huu hapa,’ au ‘Ule kule,’ kwa maana Ufalme wa Mungu umo ndani yenu.”

22 rKisha Isa akawaambia wanafunzi wake, “Wakati utafika ambapo mtatamani kuiona moja ya siku ya Mwana wa Adamu, lakini hamtaiona. 23 sWatu watawaambia, ‘Yule kule!’ Au, ‘Huyu hapa!’ Msiwakimbilie. 24 tKwa maana kama vile umeme wa radi umulikavyo katika anga kuanzia mwisho mmoja hadi mwingine, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu katika siku yake. 25 uLakini kwanza itampasa kuteseka katika mambo mengi na kukataliwa na kizazi hiki.

26 v“Kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku za Mwana wa Adamu. 27 wWatu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, mpaka siku ile Nuhu alipoingia katika safina. Ndipo gharika ikaja na kuwaangamiza wote.

28 x“Ndivyo ilivyokuwa katika siku za Lutu: Watu walikuwa wakila na kunywa, wakinunua na kuuza, wakilima na kujenga. 29 yLakini siku ile Lutu alipoondoka Sodoma, ikanyesha mvua ya moto na kiberiti kutoka mbinguni ukawaangamiza wote.

30 z“Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile Mwana wa Adamu atakapofunuliwa. 31 aaSiku hiyo, mtu yeyote aliye juu ya dari ya nyumba yake, hata vitu vyake vikiwa ndani ya hiyo nyumba, asishuke kuvichukua. Vivyo hivyo mtu aliye shambani asirudi nyumbani kuchukua chochote. 32 abMkumbukeni mke wa Lutu! 33 acMtu yeyote anayejaribu kuyaokoa maisha yake atayapoteza, na yeyote atakayeyapoteza maisha yake atayaokoa. 34 adNawaambia, usiku huo watu wawili watakuwa wamelala kitanda kimoja; naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa. 35 aeWanawake wawili watakuwa wanasaga nafaka pamoja; naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa. [ 36Wanaume wawili watakuwa wanafanya kazi pamoja shambani; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.]”

37 afKisha wakamuuliza, “Haya yatatukia wapi Bwana?”

Akawaambia, “Pale ulipo mzoga, huko ndiko tai watakapokusanyika.”
Copyright information for SwhKC